Apr 24, 2017 15:05 UTC
  • Watu saba wauawa katika hujuma za kigaidi nchini Nigeria

Watu wasiopungua saba wameuawa katika hujuma mbili za kigaidi kaskazini mwa Nigeria katika jimbo la Borno ambalo ni ngome ya kundi la kigaidi la Boko Haram.

Duru za usalama Nigeria zinadokeza kuwa kumejiri milipuko miwili, mmoja katika kijiji cha Shuwari na mwingine katika barabara ya Maiduguri-Damboa-Biu ambapo magaidi watatu waliokuwa wamejifunga mishipi ya mabomu waliangamia huku wakiwaua raia wanne katika mashambulizi hayo ya Jumatatu. 

Kamishna wa Polisi katika jimbo la Borno Damian Chukwu, ametoa taarifa na kuthibitisha kutokea hujuma hizo za kigaidi mapema leo alfajiri. Amesema magaidi walijiripua wakati walipokaribia kukamatwa na maafisa wa polisi waliokuwa wakilinda doria.

Magaidi wa Boko Haram

Tokea Boko Haram ianzishe uasi wake Nigeria mwaka 2009, watu zaidi ya elfu 20 wamepoteza maisha kutokana na hujuma za kundi hilo la magaidi wakufurishaji nchini Nigeria na pia katika nchi jirani za Cameroon, Niger na Chad. Aidha zaidi ya watu milioni mbili wamefanywa wakimbizi kufuatia ugaidi wa Boko Haram.

Neno Boko Haram kwa lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Kundi hilo la Boko Haram ambalo lina ufahamu usio sahihi na potovu kuhusu dini ya Kiislamu, limekuwa likitekeleza hujuma katika maeneo mbalimbali ya Nigeria hasa kaskazini mwa nchi hiyo.

Tags