AI: Askari wa Sudan Kusini wamewaua kwa makusudi raia 60
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International (AI) limelituhumu jeshi la Sudan Kusini kwamba limefanya uhalifu wa kivita kwa kuwakosesha pumzi kwa makusudi makumi ya raia waliorundikwa katika kontena la kusafirisha bidhaa lililokuwa na joto kali.
Ripoti iliyotolewa jana na Amnesty International imesema kuwa, wahusika wa uhalifu huo wa kivita, ambao ulifanyika katika uwanja wa Kanisa Katoliki katika mji wa Leer kwenye Jimbo la Unity Oktoba iliyopita, ni lazima wafikishwe mahakamani na kukabiliwa na mashtaka. Ripoti hiyo imetegemea ushahidi wa makumi ya watu waliowaona wahanga hao wakiingizwa kwenye kontena huku mikono yao ikiwa imefungwa au walioona maiti zao zikitolewa kwenye kontena hilo.
Mashahidi wamesema walisikia sauti za wahanga hao wakilia na kupiga mayowe kwa dhiki na kugonga kuta za kontena hilo ambalo halikuwa na dirisha au sehemu nyingine ya kuingizia hewa. Ripoiti hiyo imesisitiza kuwa maafisa wa jeshi la Sudan Kusini walijua kwamba mahabusi hao wako katika dhiki na wanafariki dunia lakini hawakuchukua hatua yoyote ya kuwaokoa.
Shirika la Amnesty International limesema kuwa watu waliouawa katika kontena hilo walikuwa wafugaji, wafanyabiashara na wanafunzi na wala hawakuwa wapiganaji.
Mauaji hayo ya kutisha yaliripotiwa kwa mara ya kwanza mwezi uliopita na kamisheni ya pamoja inayosimamia usitishaji vita nchini Sudan Kusini (JMEC).
Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake za zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba amehusika na jaribio la kupindua serikali yake.