Waislamu wa Nigeria walalamikia kuendelea kushikiliwa Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu
-
Sheikh Ibrahim Zakzaky
Msemaji wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amelaani kuendelea kushikiliwa kinyume cha sheria kiongozi wa harakati hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Katika taarifa yake maalumu, Ibrahim Musa, msemaji wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema: "Siku 500 zimepita tokea aanze kushikiliwa kinyume cha sheria Sheikh Ibrahim Zakzaky, na hadi hivi sasa wakuu wa serikali hawajatoa jibu lololte kuhusu hatua yao hiyo."
Aidha amesema, Mahakama ya Fiderali ya Nigeria karibu miezi minne iliyopita ilitoa hukumu na kusema Sheikh Zakzaki anashikiliwa kinyume cha sheria na kuitaka serikali imuachulie huru mara moja lakini utawala wa Rais Muhammadu Buhari umekataa kumuachiliahuru mwanazuoni huyo wa Kiislamu.
Ibrahim Mussa ameongeza kuwa, tokea mwezi Aprili mwaka 2016, Sheikh Zakzakyi hajaruhusiwa kuonana na mawakili wake jambo ambalo pia ni kinyume cha katiba ya nchi hiyo.
Itakumbukwa kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky akiwa na mke wake walitekwa nyara na jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 katika kituo cha kidini huko mjini Zaria katika jimbo la Kaduna. Tokea wakati huo Sheikh Zakzaky na mkewe wamekuwa wakizuiliwa katika mojawapo ya vituo vya kijeshi vya nchi hiyo bila ya kufunguliwa mashkta.
Jeshi hilo lilidai kwamba, wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria walikuwa na njama ya kutaka kumuua Mkuu wa Jeshi la Nigeria, madai ambayo yamekanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo.
Jeshi hilo katili liliizika miili ya Waislamu waliouawa katika kaburi moja la umati kwa lengo la kuficha ushahidi wa ukubwa wa jinai hiyo. Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo huku Sheikh Zakzaky, ambaye hali yake ya kiafya si nzuri, akiendelea kushikiliwa korokoroni pasina kufunguliwa mashtaka.