Katibu Mkuu wa UN: Viongozi wa Afrika msing'ang'anie madaraka
-
UN Secretary General
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amewaambia viongozi wa Afrika kuwa haipasi kutumia mianya ya kisheria au mabadiliko ya Katiba yasiyo ya kidemokrasia ili "kung'ang'ania madaraka", na kwamba wanapaswa kuheshimu kikomo cha muhula wa kubakia madarakani.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameyasema mjini Addis Ababa, makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) wakati akihutubia kikao cha siku mbili cha viongozi wa nchi 54 wanachama wa umoja huo.
"Haipasi katu viongozi kutumia mabadiliko yasiyo ya kidemokrasia ya Katiba na mianya ya kisheria kung'ang'ania kubakia madarakani. Sote tumeyaona matokeo ya kimaafa walipofanya hivyo", amesema Katibu Mkuu wa UN akiwahutubu viongozi wa nchi za Afrika. Aidha amesema lazima viongozi wawalinde raia wao na si kujilinda wao wenyewe na akawapongeza viongozi waliong'atuka madarakani na kuheshimu ukomo wa muhula wa uongozi kama ulivyoainishwa kikatiba.
Viongozi kadhaa wa nchi za Kiafrika wamekuweko madarakani kwa miongo kadhaa sasa huku baadhi yao wakibadilisha Katiba ili kuweza kuendelea kutawala, na wengine wakituhumiwa kuwa na mpango wa kuondoa vikomo vya muhula wa uongozi.
Mjadala kuhusu kikomo cha muhula wa urais umezidi kupamba moto baada ya kuchochea machafuko katika baadhi ya nchi za Afrika zikiwemo Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Moja ya ajenda kuu za kikao cha viongozi wa Umoja wa Afrika ni kujadili mgogoro wa Burundi, ambako machafuko yalizuka baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza azma wa kugombea urais kwa muhula wa tatu ambao wapinzani wanasema ni kinyume cha sheria kikatiba na kwa mujibu wa Mkataba wa Amani wa Arusha. Hata hivyo Nkurunziza aligombea na kushinda uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Julai mwaka jana.
Suala la kuondoa ukomo wa muhula wa urais limeshuhudiwa nchini Rwanda wakati nchini Uganda Katiba haijaweka kikomo hicho na hivyo kumpa fursa Rais Yoweri Museveni kugombea tena urais utakaofanyika mwezi ujao wa Februari licha ya kuweko madarakani kwa muda wa miongo mitatu sasa.
Kwa upande wa Tanzania, aliyekuwa rais wa nchi hiyo Jakaya Kikwete aliondoka madarakani mwaka jana baada ya kukamilisha mihula miwili ya uongozi iliyowekwa kikatiba, lakini mgombea wa chama chake CCM ambacho kinaitawala nchi hiyo kwa zaidi ya nusu karne sasa ndiye aliyeibuka mshindi katika uchaguzi wa rais.../