DRC yadhibiti ugonjwa hatari wa Ebola
Wizara ya Afya huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza kufanikiwa kudhibiti maambukizi ya ugonjwa hatari wa Ebola.
Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Oly Ilunga Kalenga amesema katika kipindi cha siku 21 zilizopita, hakuna maambukizi yoyote mapya yaliyoripotiwa nchini.
Hii ni katika hali ambayo, mwezi uliopita, Shirika la Afya Duniani WHO, lilionya kuwa, maambukizi ya ugonjwa wa Ebola kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, yanaweza kusambaa nchi nzima.
Hadi sasa, watu 20 wamethibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo hatari ambao tayari umesababisha vifo vya watu watatu katika mkoa wa Bas-Uele.
Mnamo mwaka 2014, mkurupuko wa ugonjwa huo huko Kongo DR ulidhibitiwa kwa haraka ingawa watu 49 walifariki dunia.
Itakumbukwa kuwa, watu zaidi ya 11,000 walifariki dunia kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika eneo la Afrika Magharibi mwaka 2014 hadi 2015, hususan nchini Guinea, Sierra Leone na Liberia katika mlipuko wa Ebola ulioatajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani.