Idadi ya vifo kutokana na maradhi ya Ebola DRC vyafikia 506
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i139690-idadi_ya_vifo_kutokana_na_maradhi_ya_ebola_drc_vyafikia_506
Idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimeongezeka na kufikia 506.
(last modified 2026-07-07T03:25:13+00:00 )
Jul 07, 2026 03:21 UTC
  • Vifo vilivyosababishwa na Ebola DR Congo vyapindukia 500
    Vifo vilivyosababishwa na Ebola DR Congo vyapindukia 500

Idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimeongezeka na kufikia 506.

Mamlaka za afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) zimetangaza kwamba idadi ya vifo kutokana na Ebola aina ya Bundibugyo imefikia 506.

Ripoti iliyochapishwa jana ilisema, kufikia tarehe 4 Julai 2026, jumla ya visa 1,561 vilivyothibitishwa viikuwa vimerekodiwa tangu mlipuko huo utangazwe tarehe 15 Mei. Hivi sasa, wagonjwa 628 wametengwa au wamelazwa hospitalini katika majimbo matatu ya mashariki mwa nchi hiyo.

Mkoa wa Ituri umeendelea kuwa kitovu cha mlipuko wa ugonjwa huo, ukichangia zaidi ya 90% ya visa vyote vilivyothibitishwa. Mkoa huo unafuatiwa na Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

Idadi jumla ya watu katika majimbo matatu yaliyoathiriwa inakadiriwa kuwa karibu milioni 15. Maafisa wa afya wana wasiwasi hasa kuhusu maeneo 36 ya afya yenye hatari kubwa, ambayo yanashuhudia uhamaji mkubwa wa watu.

Uhamaji huo mkubwa unasababishwa hasa na watu waliokimbia makazi yao ndani ya nchi wakikimbia mapigano ya makundi ya waasi na vikosi vya serikali, pamoja na uhamaji mkubwa unaohusishwa na shughuli zisizo rasmi za uchimbaji dhahabu katika eneo hilo.

Wiki saba baada ya mlipuko, juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa vifaa vya Kuzuia na Kudhibiti Maambukizi (IPC), ikiwa ni pamoja na Vifaa vya Kinga Binafsi (PPE) na klorini.

Kuna visa 96 vilivyothibitishwa miongoni mwa wafanyakazi wa afya, 19 kati yao wamefariki.

Ufuatiliaji wa watu waliogusana na wagonjwa unaongezeka kwa kasi, huku watu 10,079 wakiorodheshwa.