Washukiwa waliojiunga na Boko Haram wachunguzwa
Jeshi la Nigeria linawachunguza watu wanaoshukiwa kujiunga na kundi la kigaidi la Boko Haram nchini humo.
Lucky Irabor, Kamanda wa oparesheni iliyopewa jina la "Lafiya Dole" huko kaskazini mashariki mwa Nigeria amesema kuwa, baadhi ya wafungwa wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram hivi karibuni watafikishwa mahakamani. Irabor ameongeza kuwa, aghalabu ya waliotiwa mbaroni katika upekuzi uliofanywa na jeshi la Nigeria wamekiri kushiriki katika mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram.
Hadi kufikia sasa watu wasiopungua elfu 20 wameuliwa na wengine zaidi ya milioni mbili na laki sita wamekimbia makazi yao tangu kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram lianzishe mashambulizi na ukatili wake huko kaskazini mashariki mwa Nigeria mwaka 2009. Aidha mashambulizi ya kundi hilo la kitakifiri yameenea huko Chad, Niger na Cameroon kuanzia mwaka 2015.