Umoja wa Mataifa: Maradhi ya kipindupindu yameenea kila kona ya Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i30262-umoja_wa_mataifa_maradhi_ya_kipindupindu_yameenea_kila_kona_ya_yemen
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, maradhi ya kipindipindu yameenea katika kila kona ya Yemen huku hali ya kibinadamu katika nchi hiyo ikiripotiwa kuzidi kuwa mbaya siku baada ya siku.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 09, 2017 23:26 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Maradhi ya kipindupindu yameenea kila kona ya Yemen

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, maradhi ya kipindipindu yameenea katika kila kona ya Yemen huku hali ya kibinadamu katika nchi hiyo ikiripotiwa kuzidi kuwa mbaya siku baada ya siku.

Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen ametangaza kuwa, maradhi hayo yameenea kwa kasi na kwamba, maeneo yote ya nchi hiyo kwa sasa yamekumbwa na maradhi ya kipindupindu.

Jimmy McGoldrick amebainisha kuwa, takribani watu elfu 90 wanaugua maradhi ya kipindupindu nchini Yemen na kwamba, hadi sasa watu 700 wameshafariki dunia dunia kwa maradhi hayo.

Stephen O'Brien

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Mei, Stephen O'Brien, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura aliliambia Baraza la Usalama la umoja huo kwamba, Yemen inakaribia kusambaratika kikamilifu huku ikiendelea kukabiliwa na uvamizi wa umwagaji damu ulioanzishwa na Saudi Arabia na kukumbwa na baa la njaa na mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu, huku dunia ikiwa inatazama tu.

Kuendelea mashambulizi ya anga ya Saudia na waitifaki wake katika miundombinu, hospitali, shule na makazi ya raia na kadhalika mzingiro wa kila upande wa nchi hiyo vamizi dhidi ya Yemen, umepelekea kuenea kwa kasi maradhi kama kipindupindu na magonjwa mengine yanayoteketeza roho za wananchi wa Yemen hususan watoto.

Raia zaidi ya elfu 12  wa Yemen wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika uvamizi huo wa kijeshi huku Umoja wa Mataifa ukishindwa kuchukua hatua yoyote ya kuzuia jinai hizo za Saudia huko Yemen.