Mamia ya Wahamiaji wanyanyaswa na kushikiliwa bila ridhaa yao Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i30490-mamia_ya_wahamiaji_wanyanyaswa_na_kushikiliwa_bila_ridhaa_yao_libya
Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM limebainisha wasi wasi kuhusu hali ya takribani wakimbizi na wahamiaji 260 wa Somalia na Ethiopia wakiwemo watoto wanaoshikiliwa na wasafirishaji haramu wa binadamu au magenge ya wahalifu nchini Libya bila ridhaa yao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 15, 2017 02:51 UTC
  • Mamia ya Wahamiaji wanyanyaswa na kushikiliwa bila ridhaa yao Libya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM limebainisha wasi wasi kuhusu hali ya takribani wakimbizi na wahamiaji 260 wa Somalia na Ethiopia wakiwemo watoto wanaoshikiliwa na wasafirishaji haramu wa binadamu au magenge ya wahalifu nchini Libya bila ridhaa yao.

Kwa mujibu wa IOM picha za video zilizosambazwa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook Juni 9 zinawaonyesha mamia ya watu hao waliodhalilishwa na kuteswa wakiwa wamekusanywa kwenye chumba kidogo huku wakiwa na hofu kubwa. Inawezekana pia kuna raia wa mataifa mengine.

Wahamiaji na wakimbizi hao wameelezea madhila yanayowasibu kukiwemo kupigwa, kuteswa, wengine hata kutolewa meno, kuvunjwa mikono na kunyimwa chakula.

Wamesema wanawake wametenganishwa na wanahofia huenda wanateswa zaidi na hata kufanyiwa ukatili wa kingono. Wazazi na jamaa wa wakimbizi na wahamiaji hao pia wamekuwa wakitumiwa vipande vya video vya ndugu zao kupitia mitandao ya kijamii na kutakiwa kulipa kati ya dola 8000 hadi 10,000 au jamaa zao wauawe.

Naye mkurugenzi wa UNHCR kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini Amin Awad, amesema shirika hilo linaungana na IOM kutaka kujua mustakhabi wa wakimbizi na wahamiaji hao na kutoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa ushirikiano na serikali ya Libya.

Boti ya wahamiaji ikizama

Kwa mujibu wa IOM, watu wanaofanya biashara haramu ya magendo ya wahajiri wanatengeneza faida ya dola bilioni 35 za Marekani kwa mwaka pasina na kujali namna wanavyohatarisha maisha ya maelfu ya wahajiri.

Mwaka uliopita pekee, wahajiri zaidi ya elfu tano aghlabau wakiwa raia wa nchi za Nigeria, Eritrea, Somalia, Sudan, Gambia, Senegal, Mali, Morocco na Tunisia walifariki dunia kwa kuzama katika bahari ya Medittaraenia wakiwa katika safari hizo hatari za kuelekea Ulaya, kwenda kutafuta kazi na maisha mazuri.