Zarif: Hakuna kizuizi cha kuimarisha uhusiano wa Iran na Tunisia
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hakuna kitu kinachoweza kuzuia au kukwamisha kuimarisha uhusiano wa pande mbili wa Iran na Tunisia.
Mohammad Javad Zarif aliyasema hayo jana Jumatatu katika mazungumzo yake na Rais wa Tunisia, Beji Caid Essebsi katika mji mkuu wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, Tunis.
Amefafanua kuwa: "Tunaamini kwamba nchi mbili hizi zina fursa na uwezo wa kuimarisha uhusiano wa pande mbili; na Tehran ipo tayari kubailishana uzoefu wake katika nyuga mbalimbali na Tunis."
Sambamba na kuishukuru serikali na taifa la Tunisia, Dakta Zarif amemkabidhi Rais wa Tunisia waraka kutoka kwa mwenzake wa Iran, Hassan Rouhani.

Kwa upande wake, Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia amesema nchi yake iko tayari kupanua wigo wa uhusiano wa pande mbili na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kila nyuga akisisitiza kuwa Iran ni taifa lenye ustaarabu.
Kadhalika ametumia fursa ya mazungumzo yake na Dakta Zarif kutoa mkono wa pole kufuatia shambulizi la kigaidi la mjini Tehran la Juni 7 ambapo makumi ya watu waliuawa na kujeruhiwa, baada ya magaidi kushambulia maeneo ya Bunge la Iran na Haram ya Imam Khomeini (MA).
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alianza ziara ya kuzitembelea nchi tatu za kaskazini mwa Afrika za Algeria, Mauritania na Tunisia Jumapili iliyopita.
