Jun 26, 2017 03:33 UTC
  • Kuanza tena mazungumzo ya amani baina ya serikali ya Mali na waasi

Serikali ya Mali na makundi ya waasi nchini humo wamenza tena ya mazungumzo ya amani kutokana na kuongezeka kwa machafuko na ukosefu wa amani katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Mwaka 2015 serikali ya Mali na waasi wa nchi hiyo walitia saini makubaliano ya amani kwa shabaha ya kukomesha machafuko na vita vya ndani katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo lakini mazungumzo ya jinsi ya kutekeleza makubaliano hayo yalisimamishwa hapo baadaye. Hata hivyo kushadidi machafuko na mashambulizi ya kigaidi kumeifanya serikali ya Bamako ianze tena mazungumzo hayo ya jinsi ya utekelezaji wa makubaliano ya amani.

Mjumbe wa serikali ya Mali katika mazungumzo hayo Muhammad Mitali amesema, hamu ya waasi ya kutaka kujiunga na makundi ya kigaidi vimeifanya serikali ya Bamako ichukue uamuzi wa kujadili suala la utekelezaji wa makubaliano ya amani na pande zote zilizotia saini makubaliano hayo.

Baadhi ya makundi yanayoshiriki mazungumzo

Mapigano ya ndani nchini Mali hususan katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo yanaendelea kwa miaka kadhaa sasa. Makundi ya waasi yalitwaa udhibiti wa maeneo hayo mwaka 2012. Baada ya kushadidi mapigano katika maeneo hayo, mwezi mei mwaka 2015 serikali ya Mali na makundi ya waasi walitia saini makubaliano ya amani baada ya mazungumzo ya muda mrefu huko Algeria. Baada ya makubaliano hayo wananchi wa Mali walikuwa na matumaini ya kushuhudia amani na usalama nchini humo lakini makundi yaliyotia saini makubalino hayo hayakuheshimu vipengee vyake na yamekuwa yakiendeleza mashambulizi na mapigano katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Mazungumzo hayo yakiendelea

Kwa sasa makundi mbalimbali ya waasi yanapigana na serikali ya Bamako. Miongoni mwa makundi hayo ni lile la Harakati ya Ukombozi wa Azawad na lile la watu wa kaumu ya Toareg. Ghasia na machafuko yanayoendelea katika nchi kadhaa jirani za kaskazini mwa Afrika kama vile Libya yamekuwa sababu ya kuenea harakati na makundi ya kigaidi katika eneo hilo hususan katika nchi zinazosumbuliwa na hitilafu na machafuko ya kisiasa. Kwa mfano tu siku kadhaa zilizopita askari usalama wa Mali waliwatia nguvuni magaidi wawili waliokuwa na lengo la kushambulia maeneo ya wageni mjini Bamako. Watu hao wawili ni raia wa Mali wakazi wa maeneo yenye ghasi na machafuko ya kaskazini mwa nchi hiyo. Watu hao wawili pia ni wanachama wa kundi la kigaidi lenye mfungamano na al Qaida. Kundi hilo ndilo lililofanya shambulizi na kujilipua kwa mabomu tarehe 18 Januari katika mji wa Gao ambalo liliua zaidi ya watu 70.

Baadhi ya makundi ya waasi nchini Mali

Hii ni katika hali ambayo kikosi cha askari wa Ufaransa na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wametumwa Mali ili kusaidia jitihada za kurejesha amani kaskazini mwa nchi hiyo. Mali ina umuhimu mkubwa kwa Ufaransa na askari wa nchi hiyo wamekuwa nchini Mali kwa muda mrefu sasa kwa kisingizio cha kulinda amani na usalama. Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, hali ya sasa ya Mali ni matokeo ya siasa za kikoloni za Ufaransa katika eneo hilo hususan nchini Mali. Ala kulli hal, hadi sasa kumefanyika duru kdha za mazungumzo  jinsi ya kutekeleza makubalino ya amani baina ya serikali ya Mali na makundi ya waasi. Kwa kutilia maanani hali ya sasa kuna matarajio kuwa pande zote katika mazungumzo hyo zitaingia katika mazungumzo zikielewa vyema umuhimu wake na kufanya jitihada kubwa zaidi za kuyatekeleza na hatimaye kukomesha hatari ya balaa la gaidi linaoendelea kusababisha maafa katika nchi mbalimbali kama Libya.  

Tags