Misiba ya wakimbizi yajikariri, makumi wahofiwa kufa maji pwani mwa Libya
Makumi ya watu wanahofiwa kufa maji katika maji ya pwani ya Libya katika Bahari ya Mediterania.
Gadi ya Pwani ya Libya imetangaza kuwa, imefanikiwa kuokoa wakimbizi 85 kati ya zaidi ya watu 120 waliokuwa kwenye boti iliyozama na kwamba watu wengine zaidi ya 40 hawajulikani waliko.
Wakimbizi hao wameokolewa umbali wa kilomita 10 kutoka mji wa Garabulli baada ya boti moja ya uvuvi kuwaona wakielea baharini.
Afisa wa Gadi ya Pwani mwa Libya, Muammar Mohamed Milad amesema boti waliyokuwa wakisafiria wakimbizi hao ilipasuka ikiwa majini kutokana na idadi kubwa ya abiria wake na kuanza kuzama.
Watu waliookolewa wanasema, wenzao zaidi ya 40 wakiwemo watoto wadogo, wametoweka.
Mji wa Garabulli uko umbali wa kilomita 30 kutoka Tripoli na ni mashuhuri kwa kuwa kituo kikuu kinachotumiwa na wakimbizi kuelekea Ulaya.
Jumuiya ya Kimatafa ya Wahajiri (IOM) inasema kuwa, zaidi ya wakimbizi 85,000 wamewasili Italia hadi sasa kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu na wengine zaidi ya elfu mbili wamepoteza maisha baada ya kuzama baharini.