Libya yaialika Italia katika maji yake kupambana na magendo ya binadamu
Serikali ya Libya yenye makao yake huko Tripoli mji mkuu wa nchi hiyo imezialika meli za kivita za Italia katika maji ya nchi hiyo ili kusaidia mapambano dhidi ya magendo ya binadamu. Hayo yamesemwa leo na Paolo Gentiloni Waziri Mkuu wa Italia.
Awali Fayez al Sarraj Waziri Mkuu wa Libya anayeongoza serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa yenye makao yake huko Tripoli alipinga kuwepo katika maji ya nchi hiyo kikosi cha Umoja wa Ulaya cha kupambana na magendo ya binadamu kwa jina la "Sophia" na hivyo kukwamisha jitihada za kukomesha biashara hiyo tangu kuanza kutekelezwa mwaka 2015.
Hata hivyo Waziri Mkuu huyo wa Libya baadaye alibadilisha msimamo wake siku moja baada ya kufikiwa makubaliano kati yake na Khalifa Haftar kamanda anayesimamia eneo la mashariki mwa Libya ya kusimamisha vita kwa masharti ya kuendesha uchaguzi mwakani. Waziri Mkuu wa Italia amesema kuwa siku kadhaa zilizopita Waziri Mkuu wa Libya Fayez al Sarraj alimtumia barua akiiomba serikali ya Roma iwapatie msaada wa kiufundi katika juhudi za pamoja za kupambana na magendo ya binadamu.