Mabaradhuli 43 wapandishwa kizimbani Nigeria
Watu 43 wamefikishwa mahakamani nchini Nigeria kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya ubaradhuli na mahusiano ya kingono ya jinsia moja.
40 miongoni mwao, wakiwemo watoto wadogo 12 walikiri mashtaka dhidi yao na kuachiwa huru kwa dhamana; huku mahakama ikiwanyima dhamana watuhumiwa watatu kati yao. Iwapo watapatikana na hatia, huenda watahukumiwa kifungo cha hadi miaka 14 jela.
Mwanasheria Mkuu, Adeniji Kazeem amesema kufunguliwa mashtaka mabaradhuli hao kunalenga kusimamisha wimbi la uozo huo, haswa kwa kuwashirikisha watoto wenye umri chini ya miaka 18.
Mwaka 2014, Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria alipasisha kuwa sheria, muswada wa kupiga marufuku ubaradhuli na mahusiano ya kingono ya watu wenye jinsia moja licha ya mashinikizo kutoka kwa serikali za Magharibi.
Nchi nyingi za Afrika zinatambua maingiliano ya kingono kati ya watu wenye jinsia moja kuwa ni kosa la jinai.
Novemba mwaka jana, serikali ya Zimbabwe ilisema katu haitokubali wito wa Umoja wa Mataifa wa kukubali liwati na ndoa za jinsia moja katika nchi hiyo ya Kiafrika, miezi michache baada ya Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo kukiambia kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa, nchi yake kamwe haiwezi kuruhusu uhanithi licha ya mashinikizo kutoka nchi za Magharibi na kusisitiza kuwa, haki za mashoga sio haki za binadamu kwa kuwa zinakinzana na mila, utamaduni, desturi na thamani za ubinadamu.
Mwezi huo huo wa Novemba 2016, katika hatua iliyoonekana ni ya kupiga vita kwa dhati na kukabili jitihada za kueneza vitendo vya liwati nchini Tanzania, serikali ilifanikiwa kuidhibiti Asasi ya Kimataifa ya UPR Info, iliyoandaa mpango wa kuwashawishi maofisa wa serikali na wabunge kuunga mkono harakati za ushoga nchini humo.
Katika miaka ya hivi karibuni, nchi kama Senegal, Burundi na Sudan Kusini zilipasisha sheria zinazotambua maingiliano kama hayo kuwa ni kosa la jinai.