Raia wa Nigeria wataka kuachiwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32738-raia_wa_nigeria_wataka_kuachiwa_huru_sheikh_ibrahim_zakzaky
Wakazi wa mji wa Abuja, mji mkuu wa Nigeria wamefanya maandamano ya amani na kupaza sauti wakitaka kuachiwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu anayeendelea kushikiliwa na vyombo vya usalama nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 05, 2017 09:09 UTC
  • Raia wa Nigeria wataka kuachiwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky

Wakazi wa mji wa Abuja, mji mkuu wa Nigeria wamefanya maandamano ya amani na kupaza sauti wakitaka kuachiwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu anayeendelea kushikiliwa na vyombo vya usalama nchini humo.

Taarifa kutoka Nigeria zinasema kwamba, mamia ya Waislamu wa nchi hiyo kwa mara nyingine wamefanya maandamano ya amani mjini Abuja ambapo wamesisitiza udharura wa serikali ya Nigeria kuheshimu sheria na hukumu ya mahkama ya nchi hiyo iliyotaka kuachiwa huru kiongozi wao. Katika maandamano hayo Waislamu wameonyesha hasira zao kuhusu madai ya serikali kwamba eti hali ya Sheikh Ibrahim Zakzaky ni nzuri na kuongeza kuwa, madai hayo ni ya uongo.

Maandamano ya amani ya raia wa Nigeria yamefanyika katika hali ambayo, asasi za kutetea haki za binadamu zimearifu kuwa, hali kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky ni mbaya na zimeionya serikali kuhusiana na suala hilo.

Waislamu wa Nigeria wakiwa katika maandamano yao ya amani

Mohammad Musa Abdullahi, mmoja kati ya wajumbe wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria amesema kuwa, mwenendo mbaya wa serikali dhidi ya Sheikh Ibrahim Yaqoub Zakzaky na wafuasi wake unakiuka kikamilifu haki zao za kiraia. 

Itakumbukwa kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky alitiwa nguvuni na jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 baada ya kuvamia makazi yake na kufanya mauaji makubwa dhidi ya Waislamu. Hata hivyo licha ya mahakama za nchi hiyo kutoa hukumu ya kutaka kuachiwa huru shakhsia huyo, bado vyombo vya usalama vya Nigeria vimeendelea kumshikilia katika korokoro isiyojulikana huku ripoti zikifichua kwamba hali yake ya kiafya ni mbaya.