Der Spiegel: Mazingira ya kambi za wakimbizi Libya ni mabaya sana
Imeelezwa kuwa, mazingira yanayotawala katika kambi za wakimbizi nchini Libya ni mabaya sana.
Hayo yameelezwa na gazeti mashuhuri la Ujerumari la Der Spiegel ambalo limeripoti kwamba, hali katika kambi za wakimbizi hao ni mbaya na ya kutisha.
Ripoti iliyochapishwa na gazeti hilo la Ujerumani inaeleza kwamba, kambi zenye wakimbizi waliowasili nchini Libya wakiwa njiani kuelekea barani Ulaya hazina mazingira mazuri ya kibinadamu na kwamba, jambo hilo limeungwa mkono na wanadiplomasia wa Ulaya waliotembelea kambi hizo hivi karibuni.
Baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa, mazingira ya kiafya katika vituo na kambi hizo za wakimbizi ni mabaya na hayafai kwa maisha ya mwanadamu. Wanadiplomasia wa Ulaya wameutaka Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa kushughulikia hali ya wakimbizi hao ili kuzuia wakimbizi zaidi kuvuka maji ya Bahari ya Mediterania.
Mwaka jana zaidi ya wahajiri 5,000 hususan wa Kiafrika walipoteza maisha kwa kuzama katika bahari ya Mediterania wakiwa katika safari hizo hatari za kuelekea Ulaya.
Libya ilitumbukia katika machafuko tangu Muungano wa Kijeshi wa NATO ulipoingia kijeshi nchini humo mwaka 2011 katika operesheni za kumpindua kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi.