Wasichana zaidi ya 100 wa Chibok warejea uraiani salama
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i33326-wasichana_zaidi_ya_100_wa_chibok_warejea_uraiani_salama
Serikali ya Nigeria imetangaza kuwa wasichana zaidi ya mia moja waliokuwa wametekwa nyara na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram mwaka 2014 sasa wako tayari kurejea katika maisha ya kawaida baada ya kupata matibabu na huduma za kisaikolojia.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Aug 18, 2017 22:02 UTC
  • Wasichana zaidi ya 100 wa Chibok warejea uraiani salama

Serikali ya Nigeria imetangaza kuwa wasichana zaidi ya mia moja waliokuwa wametekwa nyara na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram mwaka 2014 sasa wako tayari kurejea katika maisha ya kawaida baada ya kupata matibabu na huduma za kisaikolojia.

Waziri wa Masuala ya Wanawake wa Nigeria, Aisha Jummai Alhassan amesema kuwa, wasichana hao wamepewa huduma za kisaikolojia na matibabu katika mji mkuu, Abuja, kama sehemu ya mpango wa serikali wa marekebisho na kurejeshwa katika maisha ya kawaida.

Ameongeza kuwa, wasichana wote 106 wamepona kikamilifu na wako tayari kuunganishwa na familia zao na jamii na kurudi shuleni."

Wasichama 270 wa shule ya Chibok huko kaskazini mwa Nigeria walitekwa nyara na kuchukuliwa mateka na wapiganaji wa kundi la kigaidi na Kiwahabi la Boko Haram mwaka 2014. Wasichana 106 miongoni mwao walikombolewa, 60 walifanikiwa kutoroka na wengine mia moja wangali wanashikiliwa na kundi hilo.

Wasichana wa shule ya Chibok wanashikiliwa na Boko Haram

Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeitaka serikali ya Nigeria kuzidisha juhudi za kuokoa wasichana na wanawake wote wanaoshikiliwa matekani na kundi la Boko haram na kuhakikisha kwamba, wanarejea mashuleni bila ya kunyanyapaliwa.