Aug 25, 2017 04:21 UTC
  • Wahanga wa mashambulizi ya Boko Haram waongezeka nchini Niger

Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, tangu yalipoanza mashambulizi ya kwanza ya genge la kigaidi la Boko Haram nchini Niger mwezi Februari 2015, karibu watu 540 imma wameuawa au kujeruhiwa au kutekwa nyara na kundi hilo la wakufurishaji.

Ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa raia 177 wa Niger wameuliwa na Boko Haram katika kipindi cha baina ya mwezi Februari 2015 na Septemba 2016.

Genge la Boko Haram halina kambi nchini Niger lakini hata hivyo tangu mwezi Februari 2015 imekuwa ikifanya mashambulizi ya hapa na pale na kusababisha hasara za roho na mali nchini humo.

Mashambulizi ya Boko Haram yamesababisha hasara kubwa

 

Kundi la kigaidi la Boko Haram lilianzisha mashambulizi yake nchini Nigeria mwaka 2009 na mwaka 2015 likapanua wigo wa mashambulizi hayo ya kigaidi hadi katika nchi jirani za Niger, Cameroon na Chad. Watu 20 elfu wanakadiriwa kuuawa katika mashambulizi ya Boko Haram na wengine zaidi ya milioni mbili kuwa wakimbizi.

Udhaifu wa majeshi ya nchi za eneo hilo hususan Nigeria na kushindwa kwao kukabiliana na mashambulizi ya mara kwa mara ya Boko Haram kumepelekea kushindwa juhudi zote za kulitokomeza kundi hilo la kigaidi.

Tags