Waislamu Nigeria walalamikia kuongezeka machafuko ya kikabila
Mjumbe mmoja wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amelalamikia kuongezeka machafuko ya kikabila katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Shirika la habari la Reuters limemnukuu Said Abubakr, mmoja wa wanachama waandamizi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria akisema hayo leo na kulaani vikali hatua ya hivi karibuni ya watu wa kabila la Igbo ya kuwapa muda maalumu vijana wa eneo la Arewa la kaskazini mwa Nigeria kuondoka kusini mwa nchi hiyo na kurejea kwao kaskazini.
Said Abubakr ni mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa katika Baraza Kuu la Masuala ya Waislamu nchini Nigeria, chombo ambacho kina taathira kubwa kwa jamii ya Waislamu nchini humo.
Machafuko ya kikabila na kidini ni mambo yanayotokea mara kwa mara nchini Nigeria.
Nchi hiyo imewahi kushuhudia machafuko makali ya umwagaji damu baina ya makabila mawili ya Igbo na Hausa tangu Nigeria ilipopata uhuru wake kutoka kwa mkoloni Muingereza, na inasemekana kuwa karibu watu milioni tatu waliuawa katika machafuko hayo makali sana.