Mlipuko wa kipindupindu waua zaidi ya watu 50 nchini Chad
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34691-mlipuko_wa_kipindupindu_waua_zaidi_ya_watu_50_nchini_chad
Watu zaidi ya 50 wamepoteza maisha kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini Chad.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 22, 2017 04:16 UTC
  • Mlipuko wa kipindupindu waua zaidi ya watu 50 nchini Chad

Watu zaidi ya 50 wamepoteza maisha kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini Chad.

Hamid Djabar, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ya nchi hiyo amesema kesi zaidi ya 300 za ugonjwa huo zimeripotiwa nchini humo hadi sasa, vikiwemo vifo vya watu 52.

Amesema aghalabu ya kesi hizo zimeripotiwa katika eneo la Sila, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Sudan na Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Afisa huyo wa Wizara ya Afya ya Chad ameongeza kuwa, kesi 19 vikiwemo vifo vya watu wawili zimeripotiwa katika eneo la Salamat ingawaje anasisitiza kuwa kwa sasa hali imedhibitiwa.

Mwezi mmoja uliopita, mlipuko wa kipindupindu uliripotiwa Kongo DR

Serikali ya Chad ilitangaza habari za mlipuko huo wa kipindupindu Jumatatu iliyopita na kuunda Kamati ya Dharura inayoshirikiana na shirika la Madaktari Wasio na Mipaka na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF katika jitihada za kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo hatari, unaoua masaa machache baada ya muathiriwa kuupata.

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, watu wasiopungua 450 walifariki dunia kutokana na mlipuko mwingine wa kipindupindu nchini Chad na katika nchi nyingine za eneo la chini ya jangwa la Sahara mwaka 2011, mbali na kesi zaidi ya 17 elfu kuripotiwa.