Makumi ya wanajeshi wa Uganda waanza kuondoka Somalia
Jeshi la Ulinzi la Uganda UPDF limeanza kuondoa makumi ya wanajeshi wake wanaohudumu ndani ya Kikosi cha Askari wa Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia Amisom.
Hayo yamesemwa leo Alkhamisi na Luteni Kanali Deo Akiiki, Naibu Msemaji wa UPDF ambaye ameongeza kuwa, Uganda inapania kuondoa jumla ya wanajeshi 281 nchini Somalia kufikia Disemba 31.
Kuna zaidi ya wanajeshi 6,000 wa Uganda ambao wanatekeleza jukumu la kulinda amani nchini Somalia chini ya Amisom katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Hivi karibuni kikosi cha Amisom kilisema kimeanza kupunguza idadi ya askari wake nchini humo na kwamba kufikia Disemba 31, askari 1000 wa kikosi hicho watakuwa wameondoka katika ardhi ya Somalia.
Si vibaya kukumbusha hapa kuwa, mwezi Julai mwaka huu, askari 12 wa Uganda waliuawa katika shambulizi lililofanywa na wapiganaji wa kundi la kigaidi la al Shabab kusini mwa Somalia, siku chache baada ya serikali ya Kampala kusema itatuma wanajeshi 2000 nchini Somalia kwa ajili ya kupambana na wapiganaji wa kundi la al Shabab.
Umoja wa Afrika umesema unapania kuondoa askari wote 22 elfu wa Amisom waliotumwa nchini Somalia mwaka 2007, kufikia mwaka 2020.