Umoja wa Mataifa watahadharisha kuhusu kuteswa raia Cameroon
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37319-umoja_wa_mataifa_watahadharisha_kuhusu_kuteswa_raia_cameroon
Kamati ya Kukabiliana na Mateso ya Umoja wa Mataifa imetahadharisha kuhusu vitendo vya utesaji vinavyofanywa na wanajeshi wa serikali ya Cameroon dhidi ya raia chini ya anuani ya mapambano dhidi ya ugaidi katika maeneo ya wakazi wanaozungumza lugha ya Kiingereza.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Dec 08, 2017 00:54 UTC
  • Umoja wa Mataifa watahadharisha kuhusu kuteswa raia Cameroon

Kamati ya Kukabiliana na Mateso ya Umoja wa Mataifa imetahadharisha kuhusu vitendo vya utesaji vinavyofanywa na wanajeshi wa serikali ya Cameroon dhidi ya raia chini ya anuani ya mapambano dhidi ya ugaidi katika maeneo ya wakazi wanaozungumza lugha ya Kiingereza.

Kamati hiyo ya Umoja wa Mataifa imetaka serikali ya Cameroon kukomesha vitendo hivyo vya utesaji na kutumia mabavu dhidi ya raia hao chini ya anuani ya kuendesha mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram. Kamati ya Kukabiliana na Mateso ya Umoja wa Mataifa imetaka serikali ya nchi hiyo idhibiti utiaji mbaroni wa raia katika maeneo ya wakazi wanaozungumza lugha ya Kiingereza.  

Kamati hiyo ya Umoja wa Mataifa imeitaka serikali ya Cameroon iwazuie askari wake wa usalama kutumia mabavu kinyume cha sheria, kuteka nyara na kuwakamata raia kiholela. 

Kamati ya UN ya Kukabiliana na Mateso imeripoti kuwa watu 17 waliuawa katika ufyatuaji risasi uliofanywa na askari usalama wa Cameroon mwezi Oktoba mwaka huu, watu zaidi ya 500 wametiwa mbaroni kinyume cha sheria khususan katika hospitali na wengine 362 wamepandishwa kizimbani katika mahakama za kijeshi nchini humo kwa tuhuma za ugaidi. 

Askari usalama wa Cameroon wakiwa wakikabiliana na raia wanaotaka kujitenga 

Maeneo yanayozungumza lugha ya Kiingereza nchini Cameroon yalitumbukia katika mgogoro wa kijamii na kisiasa sambamba na kuongezeka maandamano tangu mwezi Novemba mwaka jana baada ya wakazi maeneo hayo kudhihirisha azma yao ya kutaka kujitenga.