Mar 25, 2016 03:45 UTC
  • Makamanda wawili wa Boko Haram watiwa mbaroni Nigeria

Polisi ya Nigeria imewatia mbaroni makamanda wawili wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika jimbo la Taraba, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Shaba Alkali, mkuu wa polisi wa jimbo hilo la Taraba amewataja vinara hao wa kundi hilo maarufu kwa kutenda jinai dhidi ya binaadamu kuwa ni, Ali Audu na Abdulmumini Abdullahi. Amesema kuwa, baada ya kuwatia mbaroni watuhumiwa hao, polisi imewakabidhi kwa jeshi la jimbo la Yobe la nchi hiyo. Majina ya viongozi hao wa kundi la Boko Haram, yalikuwa katika orodha ya majina ya wanachama wa genge hilo wanaotafutwa na jeshi la Nigeria kwa muda mrefu sasa. Mwaka jana jeshi la nchi hiyo lilisambaza majina ya wafuasi wa kundi hilo yakiwemo ya watuhumiwa hao wawili. Kwa akali vinara watano ambao walikuwa wakitafutwa na serikali ya Abuja, walitiwa mbaroni mwaka jana na jeshi la nchi hiyo na hivyo kupunguza kwa kiasi fulani uwezo wa kundi hilo ambalo limetangaza utiifu wake kwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.

Tags