Vikosi vya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini vyaongezewa muda
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha uamuzi wa kurefusha muda wa kuhudumu Ujumbe wa Kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS kwa miezi mitatu zaidi.
Baraza la Usalama pia limepitisha taarifa ya mwenyekiti wake kuhusu Sudan Kusini, ikionesha wasiwasi wake mkubwa kutokana na hali mbaya ya kisiasa, kiusalama, kibinadamu, haki za kibinadamu na hali ya kiuchumi nchini humo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, baraza hilo la usalama linafuatilia vitendo vya makundi hasimu yanayozozana nchini humo ambayo kwa vitendo vyao hivyo yanasababisha kuendelea hali mbaya, wakati watu milioni 7.6 wakiwa wanahitaji misaada, milioni 4 wakiwa wamekimbia makazi yao, na milioni 6 kukosa chakula.
Pia baraza hilo limewahimiza mahasimu nchini Sudan Kusini kujiunga na mchakato wa amani unaoongozwa na nchi za Afrika.
Vita vya ndani nchini Sudan Kusini vilivyoanza Disemba 2013 vimeshasababisha mauaji ya maelfu ya watu na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alifanya njama za kutaka kuipindua serikali yake.