Mawaziri wawili wa serikali iliyopita ya Zimabwe wafunguliwa mashtaka ya ufisadi
Mawaziri wawili waliohudumu katika serikali ya aliyekuwa rais wa Zimbabwe Robert Mugabe wamefunguliwa mashtaka ya ufisadi, katika kile kinachoonekana kama hatua ya kuwakandamiza maafisa waaminifu kwa Mugabe.
Waziri wa zamani wa mambo ya nje Walter Mzembi na mwenzake wa nishati Samuel Undenge jana walifunguliwa mashtaka ya "uhalifu wa kutumia vibaya mamlaka". Hayo yameelezwa na mawakili wao ambao wameongeza kuwa washtakiwa hao wawili wamekana shtaka hilo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Undenge ameshtakiwa kwa kuidhinisha mkataba wenye thamani ya dola 12,650 kwa njia ya zabuni kwa kampuni ambayo haikufanya kazi yoyote.
Mawaziri hao wawili wa serikali ya Mugabe wameachiliwa huru leo kwa dhamana na kutakiwa kukabidhi pasi zao za kusafiria hadi kesi yao itakaposikilizwa tarehe 22 Januari.
Waziri wa zamani wa Fedha Ignatius Chombo naye pia aliachiwa huru kwa dhamana baada ya kufunguliwa mashtaka mwezi Novemba kwamba alijaribu kuchukua fedha kwa njia ya udanganyifu katika benki kuu ya Zimbabwe zaidi ya muongo mmoja uliopita. Yeye Chombo pia amekana shtaka hilo.
Robert Mugabe, mwenye umri wa miaka 93 alilazimika kujiuzulu na kung'atuka madarakani mwezi Novemba mwaka jana baada ya kukaa madarakani kwa muda wa miaka 37 kufuatia mapinduzi baridi ya kijeshi yaliyomfungulia njia aliyekuwa makamu wake Emmerson Mnangagwa kushika hatamu za uongozi.
Baada ya jeshi kutwaa madaraka lilimweka kizuizini Mugabe na mkewe Grace aliyekuwa akichuana na Mnangagwa katika kuwania nafasi ya kumrithi mumewe.../