Mabalozi wa Afrika UN wapendekeza Trump akutane na viongozi wa Afrika Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39173-mabalozi_wa_afrika_un_wapendekeza_trump_akutane_na_viongozi_wa_afrika_ethiopia
Mabalozi wanaowakilisha nchi za Afrika katika Umoja wa Mataifa wamependekeza Rais Donald Trump wa Marekani akutane na viongozi wa nchi za Afrika nchini Ethiopia mwezi huu kufuatia kauli chafu aliyotoa kwamba wahamiaji wanaoingia nchini Marekani kutoka Afrika na Haiti wanatoka kwenye nchi za "shimo la kinyesi".
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 19, 2018 03:54 UTC
  • Mabalozi wa Afrika UN wapendekeza Trump akutane na viongozi wa Afrika Ethiopia

Mabalozi wanaowakilisha nchi za Afrika katika Umoja wa Mataifa wamependekeza Rais Donald Trump wa Marekani akutane na viongozi wa nchi za Afrika nchini Ethiopia mwezi huu kufuatia kauli chafu aliyotoa kwamba wahamiaji wanaoingia nchini Marekani kutoka Afrika na Haiti wanatoka kwenye nchi za "shimo la kinyesi".

Duru za kidiplomasia katika Umoja wa Mataifa zimeripoti kuwa mabalozi hao wamekutana na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley ambaye amewaeleza kwamba anasikitika kutokana na mkasa huo wa kisiasa unaolezewa kuwa ulitokea wiki moja iliyopita katika kikao kuhusu uhamiaji kilichofanyika Ikulu ya rais wa Marekani, White House.

Kwa mujibu wa wanadiplomasia, balozi wa Afrika Kusini katika Umoja wa Mataifa Jerry Matjila ambaye alizungumza kwa niaba ya kundi la mabalozi wa nchi za Afrika katika UN amemueleza Haley kwamba litakuwa "jambo la manufaa" kwa Trump kuzungumza moja kwa moja na viongozi wa Afrika wakati viongozi hao watakapokutana mjini Addis Ababa katika mkutano wa AU. Mkutano huo unatazamiwa kufanyika tarehe 28 na 29 mwezi huu.

Balozi wa Afrika Kusini UN, Jerry Matjila

Katika mazungumzo hayo na mabalozi wa Afrika, balozi wa Marekani UN amesema yeye hajui kilichosemwa katika kikao hicho cha White House lakini ameahidi kwamba atafikisha ujumbe huo wa mabalozi wa Afrika kwa Trump atakapokutana naye leo mjini Washington.

Nchi kadhaa za Afrika zimelaani kauli chafu iliyotolewa na Donald Trump kuhusiana na nchi za bara hilo huku baadhi yao zikichukua hatua ya kuwaita mabalozi wa Marekani katika nchi hizo na kuwakabidhi malalamiko yao kutokana na kejeli hizo za Trump.../