Uchaguzi mkuu Ethiopia; Abiy Ahmed anatarajiwa kushinda tena kiti cha Waziri Mkuu
Uchaguzi mkuu wa Ethiopia unatarajiwa kufanyika Jumatatu hii huku migogoro ikiendelea katika baadhi ya maeneo ya nchi, ikimaanisha kuwa watu wengi hawataweza kupiga kura.
Huu ni uchaguzi wa saba tangu kuanguka utawala wa kijeshi nchini Ethiopia mwaka 1991 – katika machafuko yaliyosababisha kujitenga Eritrea miaka miwili baadaye – na unafanyika huku uhusiano wa Ethiopia na jirani yake wa kaskazini ukikabiliwa na hatari.
Waziri Mkuu wa sasa wa Ethioia, Abiy Ahmed, anapewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda na kuchaguliwa tena kuingoza nchi hiyo- ingawa hachaguliwa moja kwa moja na wananchi. Wapiga kura nchini Ethiopia huchagua wawakilishi wao kwenye Bunge lenye viti 547, na chama kinachopata angalau viti 274 huwa na haki ya kuunda serikali ijayo ili kuongoza nchi kwa miaka mitano ijayo.
Mabango ya kampeni yenye picha za Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, kutoka Chama cha Mafanikio (Prosperity Party) yameonekana yakiwa yametundikwa katika barabara inayoelekea mji alikozaliwa wa Beshasha katikati mwa nchi hiyo. Waziri Mkuu wa Ethiopia anatumbuliwa na wenyeji wa mji huo alikozaliwa kama shujaa.
Abiy Ahmed alizaliwa mwaka wa 1976 katika familia ya kawaida katika mji wa kijijini wa Beshasha katikati mwa Ethiopia wenye wakazi karibu 8,000, na ni shakhsiya wa kwanza kutoka jamii ya Oromo kuwahi kuiongoza Ethiopia.
Abiy, mwenye umri wa miaka 49, aliingia madarakani mwaka wa 2018 kufuatia maandamano makubwa ya kupinga serikali dhidi ya chama cha People's Revolutionary Democratic Front (EPRDF), muungano - unaoongozwa na wanasiasa kutoka Tigray - ambao ulikuwa umetawala tangu 1991.
Wakazi wa mji wa Beshasha, anakotoka Waziri Mkuu huyo, wameitaja miradi ya maendeleo katika mji huo kuwa ishara za mabadiliko.
Hata hivyo wakosoaji wanaishutumu serikali yake kwa kukandamiza upinzani, kuwalazimisha wapinzani kwenda uhamishoni na kuwafunga wapinzani wa kisiasa.
Chini ya usimamizi wa Abiy, mwaka wa 2020 serikali yake ilianzisha vita na viongozi wa Tigray katika mgogoro wa miaka miwili uliokadiriwa na mpatanishi wa Umoja wa Afrika kuwa umeua watu wapatao 600,000, jambo ambalo lilisababisha eneo hilo kukumbwa na njaa.
Kwa mujibu wa ripoti ya uhuru wa vyombo vya habari ya 2025 ya Waandishi wa Habari Bila Mipaka, Ethiopia ilishika nafasi ya 148 kati ya nchi 180.
Katika chapisho lake la Septemba 2025, Human Rights Watch pia ililaani serikali ya Ethiopia kwa kuwakamata waandishi wa habari na wataalamu wa vyombo vya habari kiholela na kutoa wito wa kukomeshwa unyanyasaji wa waandishi wa habari huru.