Sudan yazituhumu Imarati na Ethiopia kushambulia uwanja wa ndege wa Khartoum
Sudan leo Jumanne imrudisha nyumbani balozi wake nchini Ethiopia kwa mashauriano na kuzituhutumu Ethiopia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuwa zimehusika na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (droni) katika uwanja wa ndege wa Khartoum.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Mohieddin Salem amesema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Khartoum kwamba, Sudan "imemwita balozi wake nchini Ethiopia kwa mashauriano kuhusu hujuma ya ndege zisizo na rubani za Imarati na Ethiopia katika uwanja wa ndege wa Khartoum."
"Uwanja wa ndege wa Khartoum ni kituo cha kiraia, na ni marufuku kuulenga kwa mujibu wa sheria ya kimataifa," amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan.
Salem amesema kuna "ushahidi kamili" kuwa shambulio hilo limefanywa kutokea Ethiopia.
Serikali ya Sudan imesema kuwa nchi zote mbili, Ethiopia na Imarati, zinabeba dhima ya mashambulizi dhidi ya uwanja wa ndege wa Khartoum na kwamba ina haki ya kujibu.
Hadi sasa Ethiopia na Imarati hazijatoa taarifa yoyote kuhusu suala hili. Nchi mbili hizi awali zilikanusha kuhusika na mzozo wa Sudan.