Chama tawala Zimbabwe chawatimua bungeni wafuasi 11 wa Mugabe
Chama tawala nchini Zimbabwe ZANU-PF kimewafukuza bungeni waitifaki na wafuasi 11 wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Robert Mugabe, huku rais mpya Emmerson Mnangagwa akiendelea kuwatimua maafisa waliomuunga mkono hadharani Mugabe na mkewe Grace.
Japokuwa Rais Mnangagwa amekuwa akitoa kauli za kupinga ulipizaji visasi, lakini vyombo vya habari nchini Zimbabwe vinaripoti kuwa mkakati wa kukijenga upya chama cha Zanu-pf nchini kote umekuwa ukiwalenga wale waliojitokeza hadharani kumuunga mkono Mugabe na mkewe Grace.
Kwa mujibu wa taarifa za bunge, naibu spika wa bunge la Zimbabwe Mabel Chinomona amesema ZANU-PF imelitaarifu bunge kuwa wabunge hao 11 hawawakilishi tena maslahi ya chama hicho, hatua ambayo inachochea kutimuliwa bungeni.
Baadhi ya wabunge hao walikuwa mawaziri katika serikali ya Robert Mugabe. Mnamo mwezi Novemba mwaka jana, chama tawala nchini Zimbabwe kiliwatimua bungeni waitifaki wakuu watano wa Mugabe akiwemo Jonathan Moyo aliyekuwa msemaji mkuu wa mrengo uliokuwa ukiunga mkono Bi Grace awe mrithi wa kiti cha urais baada ya mumewe.
Wanasiasa wengi waliokuwa wakimuunga mkono rais huyo wa zamani wa Zimbabwe ama walitiwa nguvuni na jeshi katika kamatakamata iliyoanza tarehe 15 Novemba au walitorokea nchi jirani.../