Mkutano wa 30 wa AU, juhudi za kushinda migogoro ya Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39637-mkutano_wa_30_wa_au_juhudi_za_kushinda_migogoro_ya_afrika
Mkutano wa 30 wa Umoja wa Afrika (AU) unafanyika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa kwa kaulimbiu ya "Ushindi katika Mapambano dhidi ya Ufisadi na Mageuzi Barani Afrika".
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 29, 2018 12:10 UTC
  • Mkutano wa 30 wa AU, juhudi za kushinda migogoro ya Afrika

Mkutano wa 30 wa Umoja wa Afrika (AU) unafanyika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa kwa kaulimbiu ya "Ushindi katika Mapambano dhidi ya Ufisadi na Mageuzi Barani Afrika".

Miongoni mwa masuala yanayojadiliwa katika mkutano huo uliotazamiwa kumalizika leo ni changamoto na migogoro ya Afrika, mapambano dhidi ya ufisadi na ugaidi na kukomesha udhibiti wa kiuchumi wa nchi za nje ya bara la Afrika.

Katika kikao cha kwanza cha mkutano huo kilichofanyika jana, Rais Paul Kagame wa Rwanda alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika. 

Masuala yanayojadiliwa katika mkutano wa viongozi wa Afrika yanaweza kugawanywa katika sehemu tatu za kisiasa, kiuchumi na kiusalama. Katika upande wa kisiasa hali ya ndani katika nchi za Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yanapewa umuhimu katika ajenda ya viongozi wa Afrika. Vita na mapigano ya ndani huko Sudan Kusini ni miongoni mwa changamoto kubwa za bara la Afrika. Kumefanyika jitihada za kikanda na kimataifa kwa ajili ya kukomesha vita na mapigano ya ndani nchini Sudan Kusini lakini hadi sasa jitihada hizo hazijazaa matunda. Kwa sababu hiyo Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa Umoja wa Afrika, Moussa Faki amelaani ukati na mauaji ya kinyama yanayofanyika katika mapigano ya ndani huko Sudan Kusini na kusema: Umoja huo utawawekea vikwazo wale wote wanaokwaza na kutatiza juhudi za kurejesha amani na usalama nchini Sudan Kusini. 

Mkutano wa Umoja wa Afrika, Addid Ababa

Suala la kurejesha amani na utulivu na kupambana na ugaidi ni miongoni mwa masuala yanayopewa umuhimu makhsusi katika mkutano wa sasa wa viongozi wa Umoja wa Afrika. Machafuko ya Libya na kushindwa kundi la Daesh katika nchi za Iraq na Syria kumeiweka zaidi Afrika katika hatari ya makundi na harakati za kigaidi; kwa msingi huo kudhamini usalama na kupambana na ugaidi ni miongoni mwa mambo yanayozishughulisha fikra za nchi nyingi za Afrika. 

Katika upande wa masuala ya kiuchumi, ajenda ya mazungumzo ya viongozi wa Afrika imejumuisha suala la kupanua ushirikiano wa kiuchumi, marekebisho ya kiuchumi, kuanzisha maeneo huru ya biashara na kupambana na ufisafi na ubadhirifu wa mali ya umma. Ripoti za mashirika ya kimataifa zinasema kuwa, nchi nyingi za Afrika zinasumbuliwa na ufisadi wa kutisha, suala ambalo lina taathira nyingi mbaya za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema, kuwepo madarakani watawala madikteta na tegemezi, ushawishi na udhibiti wa nchi za kigeni na usimamiaji mbaya wa mali ya umma ni miongoni mwa sababu za kukithiri ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma katika nchi nyingi za bara hilo. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana suala la kupambana na ufisadi likapewa umuhimu katika mkutano wa sasa wa Umoja wa Afrika.

Rais mpya wa Liberia, George Weah anasema: "Ufisadi ni balaa linalozisumbua nchi zote za Afrika na linazuia ustawi na maendeleo yetu. Vilevile ufisadi unatishia amani na usalama wa nchi za Afrika, uchumi na nchi zote za kanda hii."

Ukumbi wa mkutano wa viongozi wa AU, Addis Ababa

Ingawa washiriki katika mkutano wa 30 wa viongozi wa Afrika mjini Addis Ababa wana matarajio ya kuarifisha sera mpya na hatua za kivitendo za kukomesha matatizo na changamoto nyingi za nchi za bara hilo lakini inaonekana kuwa, changamoto kubwa zaidi ya yote ni dhamana ya utekelezaji wa maamuzi yatakayochukuliwa mwishoni mwa mkutano huo.