Mapigano Ethiopia yapelekea milioni moja kuwa wakimbizi
Mapigano baina ya makabila mawili makubwa Ethiopia yamepelekea watu zaidi ya milioni moja kukimbia makao yao.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa mapigano baina ya watu wa makabila ya Oromo na Somali katika maeneo ya mipaka ya majimbo yao ambayo yalijiri mara kadhaa mwaka 2017 na kukithiri Septemba yamepelekea watu milioni moja kukimbia makazi yao. Mamia ya watu wameuawa katika mapiganoo hayo.
Takwimu za Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM zinaonyesha idadi ya waliolazimika kukimbia vita hivyo ni zaidi ya inavyodhaniwa na kwamba idadi hiyo ni kubwa kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni nchini Ethiopia.

Machafuko katika eneo la Oromiya yalianza mwaka 2015 baada ya kutekwa ardhi za wakulima na matajiri wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Wakaazi wa eneo hilo wanailaumu serikali ya Addis Ababa kuwa ndiyo iliyowasaidia mabepari na mabwanyenye kupora ardhi zao kama ambavyo wanalalamikia pia ukandamizaji wa kisiasa wanaofanyiwa na serikali hiyo.