UN: Thuluthi moja ya Warundi wanahitaji misaada ya kibinadamu
Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limesema mtu mmoja kwa kila raia watatu wa Burundi atahitaji misaada ya kibinadamu mwaka huu, hilo likiwa ni ongezeko la asilimia 20 ikilinganishwa na mwaka jana 2017.
Garry Conille, Mwakilishi wa UNDP nchini Burundi amesema kuwa, wananchi wa Burundi wamejikuta katika hali hii ya kuogofya sio tu kutoka na hali ya kijamii na kiuchumi, bali pia kutokana na migogoro ya kimaumbile.
Amesema tathmini ya hali ya kibinadamu nchini humo inaonyesha kuwa, watu milioni 3.6, ikiwa ni thuluthi moja ya idadi jumla ya wananchi wa Burundi watahitaji misaada ya kibinadamu mwaka huu, huku akiyataka mashirika ya utoaji misaada ya kibinadamu kusaidia kuinusuru hali hili ya hatari inayowakodolea macho Warundi.
Amesema Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa unakisia kuwa Burundi inahitaji dola milioni 141 za Marekani (yuro milioni 115 million) kukidhi mahitaji ya Warundi wanaohitaji misaada ya dharura na ya kibinadamu mwaka huu.
Burundi mbali na matatizo yake ya ndani, inakibiliwa na mzigo mkubwa wa wakimbizi; ambapo kufikia mwishoni mwa mwezi uliopita pekee, wakimbizi 6,692 raia wa Kongo, wanaokimbia mapigano kati ya jeshi la serikali na waasi katika mkoa wa mashariki wa Kivu Kusini waliingia nchini humo.