UN yakosoa ukandamizaji wa waandishi habari Sudan Kusini
Umoja wa Mataifa umekosoa mienendo na hatua zinazochukuliwa na serikali ya Sudan Kusini dhidi ya waandishi wa habari.
Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa imesema, tangu mwaka mmoja na nusu uliopita waandishi wa habari wameuawa, kupigwa au kutiwa nguvuni nchini Sudan Kusini.
Ripoti hiyo imesema kuwa katika kipindi hicho pia waandishi wengine wa habari wamefutwa kazi au wamezuiwa kufanya shughuli zao.
Kamanda wa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, David Shearer amesema akiwa Juba kwamba, hatua hizo za serikali ya Sudan Kusini dhidi ya waandishi habari zimekuwa na taathira mbaya kwa uhuru wa kusema na kufunga anga ya mijadala na kubadilishana mawazo.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa imewataja maafisa wa serikali ya Sudan Kusini kuwa ndio wanaohusika na ukandamizaji wa waandishi wa habari.
Sudan Kusini imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwezi Disemba mwaka 2013 baina ya jeshi la taifa linalomuunga mkono Rais Salva Kiir wa nchi hiyo na waasi wanaoongozwa na makamu wa zamani wa rais wa nchi hiyo, Riek Machar.