Waislamu Tanzania waja juu baada ya kutishiwa kuvunjwa msikiti wao + Video
Waislamu mkoani Rukwa Tanzania wamemlalamikia vikali mkuu wa mkoa huo kwa kufanya njama za kutaka kuvunja msikiti ambao umekuwa unaendelea na ujenzi kwa muda wa miaka mingi.
Akizungumza mbele ya Waislamu nje ya jengo la msikiti huo, Sheikh Mkuu wa mkoa wa Rukwa Sheikh Rashid Akilimali amesema kwamba anashangaa kwa nini wafuasi wa dini nyingine wanapewa ruhusa ya kujenga majengo yao ya ibada lakini Waislamu hawapewi.
Hasira hizo za Waislamu zimekuja kufuatia ripoti kwamba mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo ametoa amri ya kusimamishwa ujenzi wa msikiti huo na kuaamrisha mafundi kuondoka msikitini hapo.
Akizungumza mbele ya jengo la msikiti huo, Sheikh Akilimali amesema, Waislamu mkoani Rukwa wanabaguliwa na mkuu huyo mpya wa mkoa. Amesema, jengo hilo limekuwepo miaka mingi, na wakuu wa mikoa wawili wameshahudumu mkoani humo na wote hawakuzuia ujenzi wa msikiti huo.
Aidha amewataka viongozi na Waislamu mkoani Rukwa kususia kushirikiana na serikali katika jambo lolote lile na kutoa mfano akisema: “Hata leo sikwenda kwenye kikao cha RCC (kamati ya ushauri ya mkoa). Siwezi kwenda kwa mkuu wa mkoa ambaye ndiye mwenyekiti wa kikao hicho, amewadhalilisha viongozi wangu wa Kiislamu.”
Aidha amesema, mkuu wa mkoa, Joachim Wangabo ni mtu mwenye kiburi, hata viongozi wa Kiislamu walipokwenda kuzungumza naye kuhusu jambo hilo aliwajibu kijeuri, suala ambalo amesema ni kuwadhalilisha Waislamu katika nchi yao.
Waislamu hao wamempa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa muda wa hadi Jumatano kuhakikisha mafundi wanarejea na kuendelea na ujenzi wa msikiti huo. Hata hivyo hawakusema ni hatua gani zitachukuliwa na Waislamu iwapo mkuu huyo wa mkoa hatosikiliza matakwa yao.
Gazeti moja la nchini Tanzania limeandika: "Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hatua ya mkuu wa mkoa huo kuzuia ujenzi wa msikiti na kutaka kubomolewa inafuatia madai kuwa umejengwa mjini na hivyo unaleta kelele kwa watu ambao si Waislamu."