Mar 11, 2018 16:20 UTC
  • Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika atembelea Algeria

Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika yuko Algiers, mji mkuu wa Algeria kwa ajili ya kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo kuhusu masuala ya bara la Afrika.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria imethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, Moussa Faki Mahamat, yuko nchini humo kwa ajili ya ziara rasmi ya siku tatu.

Katika ziara hiyo, Mkuu wa Kamisheni ya AU ameonana na viongozi mbalimbali wa Algeria akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Abdelkader Messahel na Waziri Mkuu, Ahmed Ouyahia na kujadiliana nao masuala ya biashara huru, amani na usalama barani Afrika.

Mousa Faki Mahamat (kulia) akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria Abdelkader Messahel, mjini Algiers

 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria imesema, moja ya jenda za mazungumzo ya Moussa Faki Mahamat na viongozi wa Algeria ni mabadiliko katika muungo wa Umoja wa Afrika na namna ya kudhaminiwa fedha za kuendeshea chombo hicho kikubwa zaidi barani Afrika.

Katika mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Abdelkader Messahel, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ameipongeza nchi hiyo kwa juhudi zake za kufanikisha malengo ya mwaka 2063 ya AU.

Hata hivyo taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria haikusema iwapo Mkuu wa Kamisheni ya Afrika ataonana na Rais Abdelaziz Bouteflika wa nchi hiyo au la.

Itakumbukwa kuwa Moussa Faki Mahamat alisaidiwa na Algeria katika kampeni zake za kuwa Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika mwezi Januari 2017.

Tags