IMN: Malalamiko yataendelea mpaka Sheikh Zakzaky atakapoachiliwa huru
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) imesisitiza katika taarifa yake kwamba, maandamano na malalamiko yataendelea hadi pale kiongozi wake Sheikh Ibrahim Zakzaky atakapoachiliwa huru.
Abdallah Mussa mmoja wa viongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema kuwa, hatua ya Rais Muhammadu Buhari ya kukataa kumuachilia huru Sheikh Zakzaky licha ya mahakama kuamuru hivyo inasikitisha hasa kwa kutilia maanani kwamba, afya ya kiongozi huyo wa Kiislamu si ya kuridhisha.
Afisa huyo wa ngazi za juu wa Harakati ya Kkiislamu ya Nigeria amesema kuwa, serikali imekuwa haisemi ukweli kuhusiana na afya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Abdallah Mussa amesisitiza kuwa, wafuasi wa harakati hiyo wameapa kwamba, wataendelea na malalamiko na maandamano hadi pale serikali itakaposalimu amri na kumuachilia huru kiongozi wao huyo.
Itakumbukwa kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky akiwa na mke wake walitekwa nyara na Jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 wakati askari walipovamia kituo chake cha kidini huko katika mji wa Zaria jimboni Kaduna. Tokea wakati huo Sheikh Zakzaky na mkewe wamekuwa wakizuiliwa katika mojawapo ya vituo vya kijeshi vya nchi hiyo bila kufunguliwa mashtaka.
Uvamizi huo ulijiri baada ya Jeshi la Nigeria kudai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria walikuwa na njama ya kutaka kumuua mkuu wa jeshi hilo, madai ambayo yalikanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo.
Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo.