UN yatuma askari zaidi katika jimbo la Unity, Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i44612-un_yatuma_askari_zaidi_katika_jimbo_la_unity_sudan_kusini
Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) kimetuma makumi ya askari wa ziada katika jimbo la Unity ili kuwadhaminia usalama raia wanaolengwa katika vita kati ya askari wa jeshi la serikali na magenge ya waasi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 17, 2018 09:38 UTC
  • UN yatuma askari zaidi katika jimbo la Unity, Sudan Kusini

Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) kimetuma makumi ya askari wa ziada katika jimbo la Unity ili kuwadhaminia usalama raia wanaolengwa katika vita kati ya askari wa jeshi la serikali na magenge ya waasi.

David Shearer, Mkuu wa UNMISS amesema katika taarifa ya leo Alkhamisi kuwa, "Tunachoshuhudia nyanjani ni mauaji ya makusudi ya raia sambamba na kubakwa na kutekwa nyara wanawake na watoto wadogo katika jimbo hilo."

Taarifa ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini imeongeza kuwa, makumi ya raia wameuawa katika mapigano yaliyofanyika katika jimbo hilo katika wiki za hivi karibuni, na kwa msingi huo kimeamua kutuma wanajeshi 150 wa kulinda amani katika eneo hilo lenye utajiri wa mafuta.

Mkuu huyo wa UNMISS ameongeza kuwa, vijiji 30 vimeshambuliwa katika makabiliano hayo ya pande hasimu katika siku za hivi karibuni, na kuwalizimisha wakazi haswa waliokuwa wakiishi katika eneo la Koch kukimbilia usalama wao eneo la Leer.

Askari wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini

Kadhalika ametoa mwito wa kufikishwa mbele ya sheria wale wote wanaowashambulia raia wasio na hatia, hususan watoto wadogo wanaoishi katika kambi ya wakimbizi iliyoko karibu na kambi ya kikosi hicho cha UN jimboni Unity.

Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 baada ya miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyochochea migawanyiko ya kikabila na mzozo wa kugombania mafuta.