Uchaguzi mkuu wa Zimbabwe kufanyika tarehe 30 Julai
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i45186-uchaguzi_mkuu_wa_zimbabwe_kufanyika_tarehe_30_julai
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ametangaza kuwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo utafanyika tarehe 30 Julai.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 30, 2018 15:18 UTC
  • Uchaguzi mkuu wa Zimbabwe kufanyika tarehe 30 Julai

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ametangaza kuwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo utafanyika tarehe 30 Julai.

Rais Mnangagwa ametangaza leo kuwa uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani utafanyika nchini Zimbabwe tarehe 30 Julai.

Tangu Zimbabwe ilipopata uhuru wake mwaka 1980, uchaguzi huo wa Julai utakuwa wa kwanza kufanyika tangu aliyekuwa rais wa nchi hiyo Robert Mugabe ang'atuke madarakani.

Zaidi ya vyama 100 vya siasa vinatazamiwa kushiriki katika uchaguzi huo.

Tangu wiki iliyopita Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe (ZEC) imeanza kazi ya kuhakiki majina ya watu waliotimiza masharti ya kupiga kura.

Inakadiriwa kuwa Wazimbabwe wapatao milioni tano na laki tano wametimiza masharti ya kuwawezesha kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa tarehe 30 Julai.

Rais Emmerson Mnangagwa ameahidi kuwa uchaguzi huo utakuwa huru na wa haki na utafanyika katika anga ya uwazi chini ya uangalizi wa kimataifa.

Rais Emmerson Mnangagwa (kushoto) na aliyekuwa rais wa Zimbabwe Robert Mugabe (kulia)

Mnangagwa, ambaye aliingia madarakani mwezi Novemba mwaka jana baada ya mapinduzi baridi ya kijeshi yaliyohitimisha enzi za utawala wa Mugabe, amewaalika waangalizi kutoka Jumuiya ya Madola kwenda kushuhudia zoezi hilo la uchaguzi ikiwa ni mara ya kwanza tangu uwanachama wa Zimbabwe katika jumuiya hiyo uliposimamishwa mwaka 2002 kwa tuhuma za kuchakachua matokeo ya uchaguzi. Rais Emmerson Mngangagwa aidha amewasilisha ombi la kutaka Zimbabwe ijiunge tena katika Jumuiya ya Madola.

Wachambuzi wa siasa za Zimbabwe wanasema uchaguzi wa Julai utakuwa ni mpambano baina ya maveterani wa muongo wa 1970 wa vita vya uhuru wa Zimbabwe na kizazi cha vijana wa nchi hiyo.

Mshindani mkuu wa Rais Mnangagwa mwenye umri wa miaka 75 katika kinyang'anyiro cha urais atakuwa ni Nelson Chamisa mwenye umri wa miaka 40 anayetazamiwa kuwania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha MDC.../