Waziri wa Afya: Walioaga dunia kwa homa ya manjano Angola wamefikia 225
Waziri wa Afya wa Angola ametangaza kuwa, idadi ya watu waliopoteza maisha yao nchini humo kwa homa ya manjano imeongezeka na kufikia 225.
Luis Sambo amesema kuwa, hadi sasa kumeripotiwa kesi 1600 za homa hiyo. Waziri wa Afya wa Angola amesema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa Shirika la Afya Duniani WHO na kubainisha kwamba, homa ya manjano ambayo iliibuka nchini humo mwaka jana imeshaenea katika mikoa 16 kati ya 18 ya nchi hiyo.
Mwezi uliopita, Shirika la Afya Duniani WHO lilitangaza kwamba, watu 158 wamefariki dunia nchini Angola kutokana na homa ya manjano. Kesi ya kwanza ya ugonjwa wa homa ya manjano iliripotiwa mwezi Desemba mwaka jana katika eneo moja la mji wa Luanda ambapo watu wengi waliopatwa na ugonjwa huo unaoenezwa na mbu wanaishi katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa WHO tatizo la ukusanyaji taka nchini Angola ambalo limesababisha kuwepo kwa mirundiko mikubwa ya majaa ya taka katika maeneo ya watu masikini na vilevile huduma duni za afya ni miongoni mwa sababu za kuongezeka idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na ugonjwa huo.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha kuwa asilimia 90 ya vifo vinavyosababishwa na ugonjwa wa homa ya manjano vinatokea katika bara la Afrika.