Jeshi la Mali latuhumiwa kuua makumi ya raia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46088-jeshi_la_mali_latuhumiwa_kuua_makumi_ya_raia
Makundi ya kiraia nchini Mali yamedai kuwa jeshi la nchi hiyo limeua makumi ya raia katika eneo la Mopti, katikati mwa nchi.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Jun 20, 2018 03:02 UTC
  • Jeshi la Mali latuhumiwa kuua makumi ya raia

Makundi ya kiraia nchini Mali yamedai kuwa jeshi la nchi hiyo limeua makumi ya raia katika eneo la Mopti, katikati mwa nchi.

Hayo yalibainishwa jana Jumanne na Ibrahim Thiokari, afisa wa shirika la kiraia la Fulani Association Tabital Pulaku ambaye ameongeza kuwa, wanajeshi hao wa Mali waliua raia wasiopungua 25 katika operesheni ya wiki jana dhidi ya magenge ya kigaidi yenye mfungamano na al-Qaeda, katika kijiji cha Nantaka, jimbo la Mopti.

Serikali imethibitisha kugundua makaburi matatu ya umati katika eneo hilo, ambapo raia hao waliuawa na kisha kuzikwa na wanajeshi hao, huku Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, Tiena Coulibaly, akisema wataanzisha uchunguzi kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua za kisheria.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini humo yameeleza wasi wasi juu ya kushtadi operesheni za maafisa usalama katika eneo la Mopti, ambapo wahanga wakuu ni raia wa kabila la Fulani badala ya wapiganaji wa magenge ya kigaidi. 

Askari wa kulinda amani wa UN, pamoja na wale wa Ufaransa

Mwaka 2012 kulitokea mapinduzi ya kijeshi nchini Mali suala ambalo lililotoa fursa kwa makundi yenye silaha kuzidisha mashambulizi kaskazini mwa nchi hiyo na kuteka maeneo kadhaa. 

Askari wa Umoja wa Mataifa na wa Ufaransa walitumwa nchini Mali mwaka 2013 lakini wameshindwa kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo. Mashambulizi ya makundi yenye silaha yalifika hadi kusini mwa Mali mwaka 2015.