Watu wawili wamekufa kufuatia majeraha ya mlipuko uliotokea Zimbabwe
Watu wawili wameaga dunia Zimbabwe kutokana na majeraha waliyopata kwenye mlipuko uliotokea katika mkutano wa hadhara wa kampezi za uchaguzi huko Bulawayo siku ya Jumamosi.
Watu hao wawili walijeruhiwa katika mlipuko uliotokea muda mfupi baada ya rais Emmerson Mnangagwa kutoa hotuba kwenye mkutano huo.
Rais Mnangangwa alinusurika huku makamu wa rais Bw. Kembo Mohadi na wengine 48 wakijeruhiwa.
Rais Mnangagwa amelitaja shambulizi hili kuwa "kitendo cha woga " kilichofanywa na maadui wake, na ameahidi kuwa uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Julai 30 utafanyika kama ilivyopangwa.
Mlipuko huo ulitokea wakati rais huyo wa Zimbabwe akiondoka uwanjani hapo, baada ya kuwahutubia wafuasi wake, kuelekea uchaguzi mkuu wa Julai 30.
Tukio hilo limekwenda sambamba na mlipuko mkubwa wa bomu uliotokea pia Jumamosi katika mkutano wa Waziri Mkuu mpya wa Ethiopia, Abiy Ahmed. Inaarifiwa kwamba watu 83 walijeruhiwa huku 6 wakiwa katika hali mahututi. Ilibidi Waziri Mkuu huyo aondoshwe haraka muda mfupi baada ya kutoa hotuba yake wakati mlipuko huo unaodhaniwa kuwa wa guruneti, ulipotokea.
Maelfu walikuwa wamekusanyika katika bustani kuu ya Meskel mjini Addis Ababa katika mkutano ulioandaliwa kuiunga mkono serikali ya waziri mkuu huyo. Matukio hayo mawili ya kujaribu kuwaua viongozi wa Zimbabwe na Ethiopia yameibua hofu kuhusu usalama wa marais katika bara hilo ambalo lingali linajaribu kuimarisha misingi yake ya demokrasia na utawala bora.