Apr 08, 2016 08:00 UTC
  • Kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya Rwanda

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema siku ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya Rwanda hapo mwaka 1994 ni siku ya kutoa heshima kwa wahanga wa mauaji hayo na kuzidisha upendo kwa ajili ya kuimarisha uadilifu kote duniani.

Ban Ki-moon ameyasema hayo katika ujumbe wake uliotolewa kwa mnasaba wa kukumbuka mauaji ya kimbari ya Rwanda yaliyoanza Aprili 7 mwaka 1994. Amekumbusha kuwa siku hiyo watu wasiopungua laki nane waliuawa nchini Rwanda wengi wao wakiwa Watutsi na kusema kuwa, tukio hilo ni siku ya kukumbuka maafa ya wahanga wa jinai hiyo na kuchukua azma ya kuzuia kukariri tukio kama hilo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, njia bora zaidi ya kuwa na matumaini ya kutokaririwa mauaji ya kimbari kama ya Rwanda na ukiukaji wa haki za binadamu ni kwa wanadamu wote kuheshimu majukumu yao ya pamoja, kushirikiana na kusaidiana katika hatua za kulinda maisha ya wanadamu wanaokabiliwa na hatari. Ameongeza kuwa: Historia ya mauaji ya kimbari imeonesha mara kwa mara kwamba, hakuna eneo la dunia lenye kinga ya kukumbwa na mauaji kama hayo na tahadhari kubwa zaidi ya jambo hilo ni matamshi ya kueneza chuki yaliyoenea katika mazungumzo ya umma na katika vyombo vya habari ambayo yanalenga tabaka maalumu.

Ban Ki-moon amesema maudhui ya kumbukumbu ya mwaka huu ya mauaji ya kimbari ya Rwanda imepewa jina la "kukabiliana na aidiolojia za mauaji ya kimbari" ili serikali na taasisi mbalimbali za kijamii na kisheria kote duniani zifanye jitihada za kukabiliana na matamshi yanayochochea chuki na kulipa kipaumbele suala hilo kwa ajili ya kuondoa kabisa mazingira ya kutokea tena maafa kama hayo.

Katika mauaji ya kimbari ya Rwanda mbali na watu wasiopungua laki nane kuuliwa, wanawake laki mbili pia walibakwa na kunajisiwa. Mauaji hayo yalianza baada ya kutunguliwa ndege iliyokuwa imewabeba marais wa wakati huo wa Rwanda na Burundi iliyokuwa inakaribia kutua katika uwanja wa ndege wa Kigali. Tukio hilo lilitumiwa na Wahutu wenye misimamo mikali kama kisingizio cha kushambulia na kuua Watutsi. Mauaji hayo yalisita baada ya wapiganaji wa RPF kudhibiti mji wa kigali.

Kumukuwepo mjadala mkubwa kuhusu kesi za watuhumiwa wa mauaji hayo ya kimbari ya Rwanda ambao baadhi yao wamekamatwa na kuhukumiwa na wengine wangali mafichoni katika nchi mbalimbali. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda ni matokeo ya uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo na sera zao za kuzusha hitilafu na chuki kati ya makabila na kaumu tofauti kwa shabaha ya kutimizai malengo yao ya kikoloni.

Imepita miaka 22 sasa tangu mauaji hayo yatokee lakini bado yanatambuliwa kuwa tukio la kutisha zaidi katika karne moja ya hivi karibuni hususan katika nchi za Afrika. Hali ya ndani katika baadhi ya nchi za Afrika kama Burundi la Sudan Kusini si shwari na mauaji ya kimbari ya Rwanda yanazidisha udharura wa kuchukuliwa hatua za kukomesha machafuko katika nchi hizo ili kuzuia uwezekano wa kukariri mauaji ya kimbari kama yale ya mwaka 1994.

Katika ujumbe wake kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya Rwanda, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza tena udharura wa kuwepo uadilifu na kuwajibika na kutoa wito wa kukomeshwa fikra na aidiolojia ya mauaji ya kimbari. Matamshi haya ya Ban Ki-moon yametolewa wakati uingiliaji wa madola makubwa hususan nchi za Magharibi na za kikoloni katika masuala ya nchi mbalimbali duniani kama Syria ma Yemen ungali unazusha wimbi la moto; kwa msingi huo inaonekana kuwa dawa mjarabu ya kukomesha maafa ya sasa ya mwanadamu ni kuzilazimisha nchi za kikoloni kukomesha siasa zao za kuchochea vita na hitilafu.

Tags