Jul 24, 2018 16:24 UTC
  • UN: Wapiga kura wanatishiwa Zimbabwe kuelekea uchaguzi mkuu

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeelezea wasiwasi mkubwa ilionao kuhusu kukithiri visa vya wapiga kura kutishiwa maisha nchini Zimbabwe, baadhi yao wakilazimishwa kushiriki mikutano wa kisiasa, zikiwa zimesalia siku chache wananchi waelekee katika masanduku ya kupigia kura kuwachagua viongozi wao.

Elizabeth Throssell, msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya UN amevitaka vyombo vya usalama na vyama vya kisiasa nchini humo kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unafanyika katika mazingira huru, pasi na wapiga kura kutishiwa maisha au kuumizwa.

Katika kikao na waandishi wa habari mjini Geneva leo Jumanne, afisa huyo wa UN amesema visa hivyo vimeshtadi mno hususan katika maneo ya vijijini.

Amebainisha kuwa, wagombeaji haswa wanawake wa viti mbalimbali vya uwakilishi nchini humo wanakabiliwa na wakati mgumu wa kampeni, kwani baadhi ya shakhsia na wanasiasa wanatumia lugha za kuwadhalilisha.

Rais Emmerson Mnangagwa

Hivi karibuni maelfu ya wafuasi wa upinzani walijitokeza mabarabarani kushiriki maandamano dhidi ya chama tawala nchini humo Zanu-pf katika mji mkuu Harare, sanjari na kutaka kufanyika uchaguzi huru na wa haki.

Rais Emmerson Mnangagwa ambaye alirithi mikoba ya mtangulizi wake, Robert Mugabe, anatazamiwa kuchuana na wagombea wengine kadhaa katika kinyang'anyiro cha urais mnamo Julai 30.

Tags