Wahajiri 1,500 wameaga dunia katika bahari ya Mediterania mwaka 2018
Kwa mwaka wa tano mfululizo wahajiri wasiopungua 1,500 wameaga dunia katika bahari ya Mediterania huku njia ya baharini kati ya Libya na Italia ikitajwa kuwa ya hatari zaidi ambapo mtu mmoja huaga dunia kati ya 19 wanaotumia njia hiyo.
Uhispania ambayo imeipiku Italia ikitajwa kuwa ni njia inayopendelewa zaidi na wahajiri imekwishasajili karibu wahajiri 21,000 hadi sasa, kiwango ambacho ni zaidi ya kile cha mwaka jana. Hayo yameelezwa na Shirika la Wahajiri Duniani (IOM).
Wahajiri wasiopungua 55,000 wameingia katika pwani za nchi za Ulaya katika mwaka huu wa 2018 kiwango ambacho ni zaidi ya mara mbili ya jumla ya idadi ya wahajiri 111, 753 waliowasili Ulaya mwaka uliopita.
Shirika la IOM na UNHCR zimethibitisha kuwa zitakuwa na mkutano mjini Geneva nchini Uswisi Jumatatu wiki hii kwa lengo la kujadili njia ya pamoja ya kurahisisha shughuli za kuwanusuru wahajiri baharini. Mashirika hayo hata hivyo hayakusema ni maafisa gani wa serikali watakaoudhuria mkutano huo wa faragha.