Uchaguzi wa Rais Zimbabwe waanza, Mugabe akipa mgongo chama tawala
Mamilioni ya wananchi wa Zimabwe wameelekea kwenye masanduku ya kupigia kura katika uchaguzi wa kwanza wa rais ambao haumshirikishi kiongozi mkongwe wa nchi hiyo, Robert Mugabe tangu Zimbabwe ipate Uhuru mwaka 1980.
Zaidi ya Wazimbabwe milioni tano wamejiandikisha kushiriki katika zoezi hilo la kumchagua rais mpya na wawakilishi wao bungeni.
Vituo 10,985 vimefunguliwa nchini kote kwa ajili ya zoezi la kupiga kura katika uchaguzi wa rais unaowachuanisha wagombea 23 wakiwemo wanawake 4.
Ushindani mkubwa katika uchaguzi wa leo wa rais utakuwa baina ya Rais wa sasa wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa kutoka chama tawala cha ZANU-PF na Mchungaji Nelson Chamisa anayewakilisha chama cha upinzani cha MDC na waitifaki wake.
Inatabiriwa kuwa kuna uwezekano mkubwa uchaguzi wa leo ukaingia duru ya pili hususan baada ya Robert Mugabe kusema hatakipigia kura chama chake cha ZANU-PF na wale waliomuondoa madarakani.
Wachambuzi wa siasa za Zimbabwe wanasema Mugabe bado ana ushawishi katika siasa za nchi hiyo na anaweza kuathiri matokeo ya uchaguzi huo.
Matokeo ya uchaguzi wa leo yatatangazwa Jumamosi ijayo na iwapo hakuna mgombea atakayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura, uchaguzi wa marudio utafanyika tarehe 8 Septemba.