Watatu wauawa Zimbabwe, askari usalama wapambana na wapinzani wanaopinga matokeo ya uchaguzi
Polisi ya Zimbabwe imesema watu watatu waliuawa jana wakati askari walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa upinzani waliokuwa wakirembea mawe huku wakikituhumu chama tawala cha Zanu-PF kuwa kinajaribu kuchakachua matokeo ya uchaguzi uliofanyika siku ya Jumatatu.
Msemaji wa polisi Charity Charamba ameliambia Shirika la Utangazaji la Zimbabwe (ZBC) kuwa watu hao watatu waliouawa katika vurugu na mapigano hayo bado hawajatambuliwa.
Milio ya risasi ilisikika katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare hapo jana wakati askari, baadhi yao wakiwa wameziba nyuyso zao, ambao walikuwa wakisindikizwa na magari ya deraya na helikopta za kijeshi, walipokuwa wakiwaondoa waandamanaji mabarabarani.
Machafuko yalianza mara baada ya kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Harakati kwa ajili ya Mabadiliko ya Kidemokrasia (MDC) Nelson Chamisa na mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho kutangaza kuwa ameshinda uchaguzi huo.
Baada ya wafuasi wa upinzani kuchoma moto matairi ya magari barabarani, baadhi yao waliwashambulia askari wa kuzuia fujo karibu na makao makuu ya Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe (ZEC). Askari hao walikabiliana na wafuasi hao wa upinzani kwa kutumia gesi ya kutoa machozi na mipira ya maji.
Rais Emmerson Mnangagwa aliyegombea kwa tiketi ya chama chake cha Zanu-PF ambacho kimepata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa bunge, amesema machafuko hayo yanalenga kuvuruga uchaguzi na ameubebesha lawama uongozi wa chama cha MDC.
Huku wananchi wa Zimbabwe wakiwa wanasubiri kutangazwa matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterresh ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa na wananchi kuonyesha uvumilivu na kujiepusha na aina yoyote ile ya machafuko.../