Jeshi la Zimbabwe laamuru kufungwa maduka yote Harare, matokeo ya uchaguzi karibuni
Jeshi la Zimbabwe limeamuru kufungwa maduka yote na kuwataka watu kuondoka katika maeneo ya katikati mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Harare, siku moja baada ya watu watatu kuuawa kwa kupigwa risasi na askari usalama waliotumwa kuzima maandamano ya watu waliodai kuwa matokeo ya uchaguzi wa rais yamechakachuliwa.
Hatua hiyo imezidishwa wasiwasi kwamba jeshi la Zimbabwe lililomuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa siku nyingi wa nchi hiyo, Robert Mugabe, ndilo linaloshikia madaraka ya nchi.
Karibu maduka yote ya jiji la Harare yalikuwa yamefungwa leo na mitaa ilionekana kuwa bila ya watu isipokuwa taka na matairi yaliyochomwa moto katika ghasia za jana.
Hata hivyo, George Charamba ambaye ni msemaji wa Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amekanusha kuwa kumetolewa amri ya kuvungwa maduka ya Harare na kusema kuwa habari hizo si za kweli na kwamba zinalenga kuvuruga amani.
Wakati huo huo Kamisheni ya Uchaguzi ya Zimbabwe imetangaza kuwa matokeo ya uchaguzi wa Rais na Bunge yatatangazwa hivi karibuni. Kamisheni hiyo imekanusha madai yaliyotolewa na chama kikuu cha upinzani cha MDC kwamba imekiruhusu chama tawala cha ZANU-PF kuchakachua matokeo ya uchaguzi wa Rais.
Itakumbukwa kuwa watu watatu waliuawa katika ghasia za jana wakati jeshi lililokuwa likitawanya maandano ya wafuasi wa chama cha upinzani cha MDC waliokuwa wakidai kuwa kumefanyika udanganyifu katika matokeo ya uchaguzi wa Zimbabwe.
Machafuko hayo yalianza baada ya kiongozi wa chama cha MDC, Nelson Chamisa na mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho kutangaza kuwa ameshinda uchaguzi huo.
Ilipangwa kuwa matokeo ya uchaguzi huo yatatangazwa Jumamosi ijayo na iwapo hakuna mgombea atakayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura, uchaguzi wa marudio utafanyika tarehe 8 Septemba.