Rais Emmerson Mnangagwa atangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais Zimbabwe
Tume ya Uchaguzi nchini Zimbabwe, imemtangaza asubuhi ya leo Rais wa sasa Emmerson Mnangagwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika siku ya Jumatatu iliyopita.
Kwa mujibu wa tume hiyo, Mnangagwa ameibuka mshindi kwa kupata asilimia 50.8 za kura, huku mshindani wake Nelson Chamisa, akipata asilimia 44. 3. Jana jioni polisi nchini humo, iliwatia mbaroni wafanyakazi 16 wa ofisi za chama kikuu cha upinzani cha MDC, baada ya kuvamia ofisi za chama hicho. Awali chama cha MDC kilikuwa kimetangaza kwamba mgombea wake wa urais alikuwa ameshinda katika uchaguzi uliopita. Uchaguzi wa rais, bunge na mabaraza ya miji nchini Zimbabwe ulifanyika siku ya Jumatatu ya tarehe 30 mwezi uliopita. Taarifa iliyotolewa na jeshi la polisi Alkhamisi ya jana ilisema kuwa, hali ya mambo ni tata na hivyo likaamua kuomba msaada kwa jeshi la kusimamia ulinzi kwa ajili ya kudhamini usalama.
Katika fremu hiyo, jeshi la nchi hiyo limeamuru kufungwa maduka yote na kuwataka watu kuondoka katika maeneo ya katikati mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Harare, siku mbili baada ya watu watatu kuuawa kwa kupigwa risasi na askari usalama waliotumwa kuzima maandamano ya watu waliodai kuwa matokeo ya uchaguzi wa rais yamechakachuliwa. Ghasia hizo ziliibuka baada ya kiongozi wa chama cha MDC, Nelson Chamisa na mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho kutangaza kuwa ameshinda uchaguzi huo, huku Rais Emmerson Mnangagwa akimtaka hasimu wake huyo kuiachia Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo kumtangaza mshindi. Ilipangwa kuwa matokeo ya uchaguzi huo yatatangazwa Jumamosi ijayo na iwapo hakuna mgombea atakayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura, uchaguzi wa marudio utafanyika tarehe 8 Septemba.