Wapinzani waendelea kulalamikia matokeo ya uchaguzi Zimbabwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47326-wapinzani_waendelea_kulalamikia_matokeo_ya_uchaguzi_zimbabwe
Wapinzani nchini Zimbabwe wamendelea kufanya maandamano wakilalamikia matokeo ya uchaguzi wa Rais wa hivi karibuni yaliyompa ushindi Emmerson Mnangagwa wa chama tawala cha ZANU-PF.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 09, 2018 07:55 UTC
  • Wapinzani waendelea kulalamikia matokeo ya uchaguzi Zimbabwe

Wapinzani nchini Zimbabwe wamendelea kufanya maandamano wakilalamikia matokeo ya uchaguzi wa Rais wa hivi karibuni yaliyompa ushindi Emmerson Mnangagwa wa chama tawala cha ZANU-PF.

Wafuasi wa chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC) jana walifanya maandamano katika mji mkuu Harare wakisisitiza kupinga matokeo ya uchaguzi huo.

Wapinzani hao wanadai kuwa, matokeo ya uchaguzi huo yalitiwa mkono na kwamba, mgombea wao Nelson Chamisa ndiye aliyeibuka na ushindi na ndiye aliyepaswa kutangazwa kuwa Rais mpya wa nchi hiyo.

Maandamano ya jana ni mlolongo wa maandamano ya wapinzani ambao wamekuwa wakiyafanya katika miji mbalimbali ya Zimbabwe hususan mji mkuu Harare.

Nelson Chamisa, kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC, amekataa kuyatambua matokeo ya uchaguzi wa Rais

Vyombo vya usalama vya nchi hiyo vinatuhumiwa kwamba, vimekuwa vikitumia nguvu kupita kiasi kutawanya waandamanaji hao.

Watu sita wameripotiwa kuuawa hadi sasa katika vurugu baina ya vyombo vya usalama na waandamanaji zilizozuka Agosti Mosi mwaka huu. 

Jana Tendai Biti, mmoja wa wapinzani wakubwa wa serikali ya Zimbabwe alikamatwa kwa tuhuma za kuchochea machafuko baada ya uchaguzi ambao wapinzani wameyakataa matokeo yake.

Uchaguzi wa kwanza wa Rais baada ya miaka 37 ya utawala wa Robert Mugabe ulifanyika nchini Zimbabwe tarehe 30 Julai. Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe Rais Emmerson Mnangagwa alishinda kwa asilimia 50.8 ya kura akifuatiwa na mgombea wa chama cha MDC Nelson Chamisa aliyepata asilimia 44.3 ya kura zote.