Chamisa awasilisha hoja mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi Zimbabwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47364-chamisa_awasilisha_hoja_mahakamani_kupinga_matokeo_ya_uchaguzi_zimbabwe
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe, Nelson Chamisa jana Ijumaa aliwasilisha mahakamani hoja ya kupinga ushindi wa Rais Emmerson Mnangagwa katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 11, 2018 04:03 UTC
  • Chamisa awasilisha hoja mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi Zimbabwe

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe, Nelson Chamisa jana Ijumaa aliwasilisha mahakamani hoja ya kupinga ushindi wa Rais Emmerson Mnangagwa katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni nchini humo.

Chamisa aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba timu ya kisheria imefanikiwa kuwasilisha nyaraka za chama hicho mahakamani.

Mawakili wa chama cha upinzani cha MDC jana Ijumaa waliwasili mahakamani kabla ya kumalizika muhula wa kuwasilisha nyaraka za malalamiko ya chama hicho kuhusu madai ya kufanyika udanganyifu katika matokeo ya uchaguzi wa rais wa Julai 30. Mahakama ya Zimbabwe ina muda wa siku 14 wa kutoa uamuzi kuhusu malalamiko hayo ya upande wa upinzani.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe, Rais Emmerson Mnangagwa alishinda uchaguzi wa rais kwa kupata asilimia 50.8 ya kura akifuatiwa na mgombea wa chama cha MDC, Nelson Chamisa aliyepata asilimia 44.3 ya kura zote.

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe 

Itambukwa kuwa wapinzani nchini Zimbabwe wanadai kuwa, matokeo hayo yalitiwa mkono na kwamba mgombea wao, Nelson Chamisa ndiye aliyeshinda na hivyo alipaswa kutangazwa kuwa Rais mpya wa nchi hiyo. Hivi majuzi wafuasi wa kambi ya upinzani walifanya maandamano katika miji mbalimbali ya Zimbabwe hususan katika mji mkuu, Harare ili kuoneshwa kutoridhishwa na matokeo ya uchaguzi huo.